UTAFITI: UZITO ULIOPITILIZA UNAWEZA KULETA UGONJWA WA MIFUPA (OSTEOPOROSIS)


Shirika la habari la BBC limeripoti kwamba utafiti uliofanywa na watafiti wa Marekani umegundua kwamba watu wenye uzito uliopitiliza (Obesity) wana mafuta yaliyojificha ndani ya mifupa yao ambayo yanaweza kupelekea mifupa kuwa dhaifu na rahisi kuvunjika.

Kutokana na utafiti huo, timu ya wataalamu kutoka Chuo kikuu cha Havard (Marekani), kitivo cha Tiba, waliwafanyia Scan ya mwili watu 106 (wanaume na wanawake) wenye uzito uliopitiliza ambao kwa nje walionekana kuwa na afya njema. Matokeo ya scan hiyo yalionesha kwamba baadhi ya watu hao walikutwa na mafuta hayo yaliyojificha kwenye Ini, Misuli, tumbo, hips, mapaja na uboho (bone marrow).



Dr. Miriam Bredella, ambae alihusika kwenye kazi hiyo, alisema kwamba watu wenye umbo kama tunda la apple waliobeba uzito mkubwa kwenye maeneo yanayozunguka kiuno ndio ambao wapo hatarini kupata ugonjwa huo wa mifupa (osteoporosis).

Kwa mujibu wa BBC, takribani watu milioni tatu huko UK wanakadiliwa kuugua ugonjwa wa mifupa (Osteoporosis). Watu wengi waliogundulika kuwa na ugonjwa huo, walikutwa pia na mafuta hayo yaliyojificha kwenye uboho (bone marrow) zaidi ya kiwango cha kawaida.

Matokeo ya utafiti huo yamekuja miezi michache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuionya Dunia dhidi ya kuendelea kuongezeka kwa tatizo la watu kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi na kutaka hatua zaidi kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.

Shirika hilo lilitoa Takwimu zilizoonesha kuwa karibu asilimia 70 ya watu wazima duniani wanakabiliwa na tatizo la uzito uliopitiliza na kwamba tatizo hilo linaaza kushuhudiwa hasa kwenye mataifa ya bara la Afrika (ikiwemo Tanzania) na Amerika ya kusini, huku nchi ya Marekani ikiwa ni kinara wa kuwa na watu wengi wenye uzito uliopitiliza.

Baada ya onyo hilo la Shirika la Afya dunianiani (WHO), Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha maazimio kadhaa kupambana na tatizo la uzito uliopindukia, saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Moja ya maazimio hayo ni kuzitaka nchi wanachama kutunga sheria ya kutoza kodi kwenye vyakula na juisi ambazo zinachangia kuongeza uzito, hatua itakayosaidia wananchi kupunguza matumizi yake.




No comments:

Post a Comment