Waswahili husema, ‘nyumba ni choo’, wakiwa na
maana kuwa nyumba haiwezi kuwa kamili bila kuwa na huduma hiyo ya choo.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa choo, lakini si
kila nyumba iliyo na choo au hata zile ambazo zina huduma hiyo, basi vyoo ni
vibovu, havina hadhi. Zipo aina mbalimbali za vyoo kwa matumizi ya binadamu
katika maisha yake ya kawaida.
Vyoo vina matumizi mengi ingawa
bado watu wengi hasa katika nchi maskini na zinazoendelea ikiwamo
Tanzania wanatumia choo cha kuchuchumaa wakati wa kujisaidia, lakini mijini na
katika nchi zilizoendelea, wao hutumia vyoo vya kukaa.
Nyumba nyingi mijini na ofisi mbalimbali
zinazojengwa hivi sasa, huwekewa vyoo vya kukaa. Hata zile za zamani
zinakarabatiwa na kubadilishwa kwa kuwekewa hivi ambavyo vinaonekana vya
‘kisasa’.
Mgunduzi wa vyoo vya aina hii, Thomas
Crapper anasema kwa mtazamo wake aliona kukaa wakati wa kujisaidia ni
utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.
Hata hivyo, madaktari wanapingana naye
wakisema kujisaidia katika vyoo vya kukaa kuna madhara kiafya kwa kuwa mkao huo
unaweza kuleta matokeo mbalimbali ndani ya mwili.
Utafiti uliofanywa na mtandao wa
‘naturesplatform’ umegundua kuwa matumizi ya choo cha kukaa huweza kusababisha
matatizo mbalimbali ikiwemo kansa ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wetu wa afya wa gazeti la MWANANCHI,
Samwel Shita anasema, madhara ya vyoo vya kukaa ni makubwa kwani wakati
mwingine yanaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa kutokana na
haja kubwa kubaki kwa muda mrefu katika utumbo huo.
Shita anasema mtu anapojisaidia haja kubwa katika
choo cha kuchuchumaa, kinasaidia haja yote kutoka kwa sababu ya msukumo
unaosababishwa na mkao huo.
“Unapokaa unakuwa umekaa katika choo mwili
unakuwa umelegea, hivyo inabidi utumie nguvu kubwa kujikamua kutoa haja,
tofauti na unapochuchumaa,” anasema Shita na kuongeza:
“Matatizo huanza hapo, unapojisaidia ukiwa umekaa
na kulazimisha kujikamua unaweza kusababisha vimishipa vidogo katika utumbo
mpana sehemu ya haja kubwa ya ndani na ya nje kuvimba na maumivu makali
husababishwa na ugonjwa unaojulikana kama ‘hemorrhoid,” anasema.
Anasema ‘hemorrhoid’ ni ugonjwa ambao pia huitwa
bawasiri. Mgonjwa hupata uvimbe katika njia ya haja kubwa na hivyo kupata
maumivu wakati wa kujisaidia na haja yake mara nyingine huambatana na damu.
Aidha, anasema vyoo hivi pia vinaweza kuwa chanzo
cha magonjwa yanayotokana na shambukizi katika utumbo mpana, kitaalamu
‘Inflammatory Bowel Disease’.
“Kila binadamu anapaswa kujisaidia na kuhakikisha
haja yote imetoka na kwisha kabisa, inapobakia inaweza kusababisha maambukizi
katika utumbo mpana kwa kuwa ule ni uchafu wenye mchanganyiko wa vitu vingi,”
anasema Shita.
“Haja kubwa inapokuwa tayari imeshajitengeneza
inapaswa kutoka yote, kama itabaki kipindi kirefu inaweza pia kuleta uambukizi
katika utumbo mkubwa na hata katika kidole tumbo,” anasema Shita.
“Uchafu huu si tu unaweza kusababisha maambukizi,
lakini pia unaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa. Wote tunajua kuwa
mkusanyiko wa sumu mbalimbali mwilini unakuweka katika hatari ya kupata saratani,
hivyo tatizo hili lisipotafutiwa ufumbuzi mapema linaweza kufikia huku,”
anasema Shita.
Daktari Berko Sikirov kutoka Misri ambaye
alifanyia utafiti matumizi ya vyoo vya kukaa anasema kuwa iwapo mtu ana
tatizo la vivimbe vya ‘hemorrhoid’ linaweza kumalizika iwapo ataacha kutumia
vyoo vya kukaa.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa tatizo hili linaweza
kwisha kama litakuwa katika hatua za awali. Kwa wenye tatizo lililokomaa
watalazimika kufuata matibabu kulingana na ukubwa wake.
Dk Sikirov anaongeza kuwa mbali na kupata
vivimbe, pia mgonjwa anaweza kupata tatizo la kutokupata choo kwa muda mrefu.
Anabainisha kuwa kitendo cha haja kutoka kidogo
na nyingine kubakia husababisha kuganda katika ukuta wa utumbo na zoezi hilo
huendelea mpaka kuwa tatizo sugu.
“Haja kubwa huganda katika kuta za utumbo, hali
hii huifanya haja izunguke kwa muda mrefu na ndiyo tatizo hili huanzia hapa,”
anasema na kuongeza:
“Unapojisaidia ukiwa umekaa, ile njia ya haja
kubwa huwa kama imejifunga, inabidi utumie nguvu nyingi sasa ukiwa na tatizo
hili la kukosa haja kubwa huifanya itoke kwa uchache zaidi,” anasema Dk
Sikirov.
Aidha, anasema kupata haja kubwa mara kwa mara ni
muhimu kwa kuwa usipoitoa maana yake inazungusha sumu katika damu jambo ambalo
ni hatari kwa afya.
Anaongeza kuwa kutopata haja kubwa ni kichocheo
chenye uwezo mkubwa wa kusababisha saratani ya utumbo mkubwa na uambukizi
katika kidole tumbo.
Tafsiri ya kitabibu inasema hali ya kukosa haja
kubwa ni pale mtu anaposhindwa kuipata angalau mara tatu kwa wiki. Hata hivyo,
ili ujue afya yako ni njema unapaswa kuwa unapata haja kubwa angalau mara moja
kila siku.
Daktari Denis Burkitt aliwahi kuandika
kitabu cha maelekezo ya chakula ili kuepuka ugonjwa wa saratani. Katika kitabu
hicho alieleza namna ambavyo watu wanaweza kujikinga na saratani za aina
mbalimbali.
Akizungumzia saratani ya utumbo mpana pamoja na
kuelezea vyakula na aina ya maisha, pia aliwaasa watu kutumia choo cha kukaa
ili kujiepusha na tatizo hilo.
Anaeleza kuwa kwa Marekani pekee, watu zaidi ya
150,000 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa wa saratani ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wa Ngozi katika Chuo Kikuu cha Sayansi
ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), Profesa Kisali Pallangyo anasema matumizi ya
vyoo hivyo yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya ngozi. Profesa
Pallangyo anasema ni rahisi kuambukizwa magonjwa ya ngono na ngozi kwa urahisi
pale unapotumia vyoo vya kukaa tofauti na vile vya kuchuchumaa.
Aidha, anayataja magonjwa yanayoweza
kuwambukizwa kwa kutumia vyoo vya kukaa kuwa ni kaswende, harara, mba, kisonono,
upele na mengine.
“Mtu mwenye magonjwa ya ngozi au ya ngono,
anaweza kuyaacha katika ‘sink’ anapolikalia, hivyo ni rahisi kwa mtu mwingine
‘kuyachukua’ mara atakapokaa wakati wa kujisaidia,” anasema Prof Pallangyo.
Anasema vyoo hivi ni hatari kwa afya hasa pale
vinapotumika katika jumuiya na kuongeza kuwa ni bora kutumia vile vya kukaa ili
kujikinga na magonjwa.
Source: MWANANCHI
safi sana elimu hii
ReplyDelete