Na Rose Riwa
Habari
wasomaji wa tovuti hii, natumai hamjambo na ni wazima wa afya. Kwanza kabisa
napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uzima na afya mpaka muda huu. Taka/ uchafu zimekuwa zikizagaa katika maeneo mbalimbali katika mazingira yetu na kuchafua mazingira pia kusababisha milipuko ya magonjwa ya
kuambukizwa husasani katika kipindi cha mvua, pia uchafu umekuwa ni chanzo cha
ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukihatarisha afya za watanzania hususani watoto wadogo na mama
wajawazito. Kutokana na hali hiyo serikali kwa kushirikina na wadau mbalimbali wamekuwa wakitenga bajeti kubwa na kujikita katika kuzuia magonjwa mbalimbali yatokanayo na uchafuzi wa mazingira
na pia kutenga mafungu kwenye halmashauri ili kusafisha miji na kuhakikisha
mazingira yanakuwa safi na salama. Lakini leo napenda tuangalie takataka kwa
jicho la pili, tusiishie tu kuuona
uchafu na kuuchukia bila kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa taka katika
ngazi ya familia. Na mada ya leo itajikita katika njia mbalimbali za kupunguza,
kutumia na kutunza uchafu katika mazingira ya majumbani kwetu.
Kuna
aina kuu tatu za taka na mada hii itazungumzia
aina mojawapo inayoitwa taka
ngumu (solid waste) zinazozalishwa kutokana na shughuli mbalimbali za
majumbani. Taka ngumu majumbani ni sehemu ya maisha yetu, hatuwezi kuishi bila
kutengeneza taka katika maisha ya kila siku. Hivyo basi ni muhimu kutumia na
kutunza taka hizo vizuri ili kuepuka uchafuzi wa mazigira, milipuko ya magonjwa
mbalimbali na kufanya mazingira ya nyumba na mitaa yetu kupendeza na kuvutia. Lakini pia
taka hazina tu hasara kama wengi tunavyozifikiria, kama zitatunzwa na kutumiwa kwa usahihi zinaweza
kuwa ni suluhisho la nishati katika nyumba zetu hivyo kuongeza kipato cha
familia, kupunguza gharama za kununua nishati
na gharama za utapaji wa taka hizo .Katika nchi zilizoendelea taka ni
moja wapo ya malighafi kama malighafi nyingine ambazo zinaingizia mataifa hayo
kipato kikubwa kinachotumika katika
shughuli za maendeleo. Kwa hiyo hata Tanzania tunaweza kupata faida mbalimbali
za taka kama tutafanya yafuatayo:-
1. Kutunza vizuri taka ambazo zinaweza kutumiwa kama
malighafi kutengeneza bidhaa nyingine kama vile chupa ya plastics na vyuma
chakavu aina mbalimbali na unaweza kuviuza au kugawa kwa watu
waliojiajiri/walioajiriwa (scavengers) kwa ajili ya kukusanya malighafi hii na kutegeneza bidhaa mbalimbali hii pia huongeza kipato kwa watu waliojiajiri au
waliojiriwa katika sekta hiyo,kukupatia kipato wewe mwenyewe kama utaziuza na vilevile hupunguza kwa kiwango kikubwa kiwango cha uchafu kinachozalishwa nyumbani.
2. Kutumia uchafu unaowahi
kuharibika (decomposable waste) mfano mabaki ya chakula kuzalisha gesi asilia kwa matumizi ya nishati ya
nyumbani ,kupunguza taka zinazozalishwa nyumbani na kutumia kama mbadala
wa nishati nyumbani hivyo kuokoa kiwango cha pesa nyingi ambazo tunazitumia
kila siku kwa ajili ya matumizi ya nishati
mkaa, kuni na umeme.
3. Tumia vihifadhio(packaging material)
imara pale unapoenda sokoni au kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani,
vihifadhio hivyo maalumu kama vile vikapu vimetengenezwa kwa ajili ya matumizi
ya muda mrefu na vinadumu hivyo kupunguza uchafu wa mifuko inayotumika kwa mara
moja.
4. Ikiwa utamudu, ni vizuri pia ukanunua bidhaa kubwa
itakayotumika kwa muda mrefu kulingana na matumizi yako kama vile dumu kubwa la
sabuni za maji ili kuepuka kununua madumu madogodogo mara
kwa mara hivyo kupunguza uchafu katika nyumba yako.
5. kupika chakula nyumbani
kunapunguza kiwango cha mabaki ya vifungashio vya chakula kinachonunuliwa kwenye karatasi maalum maarufu kama aluminium (foil papers) au mifuko ya plastiki maarufu
inayotumika kufungia chips na vyakula vingine hivyo kupunguza kiwango cha
uchafu nyumbani kwako.
6. Kuchemsha maji ya kunywa nyumbani
kunatukupunguzia uchafu wa makopo/chupa
za plastiki za maji zinazonunuliwa kila siku hivyo kutupunguza mlundikano wa
uchafu nyumbani kwako.
7. Nunua bidhaa zenye uwezo wa kukaa
muda mrefu (durable products) ili kuepuka kununua bidhaa hizo mara kwa mara na
kwa kufanya hivyo utapunguza gharama za maisha na kupunguza uchafu utokanao na
mabaki ya bidhaa hizo mara baada ya matumizi.
8. Kutengeneza(repair) vifaa
mbalimbali vinavyotumika nyumbani kama kunauwekano wa kufanya hivyo na kama hautaathiri usalama wa matumizi wa kifaa hicho ili kitumike kwa muda mrefu na
kuepuka kununua vifaa vingine ili kudhibiti ongezeko la uchafu katika nyumba
yako.
9. Unaweza kutumia tena mabaki ya
bidhaa zilizochakaa kwa kazi nyingine badala ya kutupa kama vile kutumia ndoo
iliyopasuka kupandia maua na kupendezesha nyumba yako badala ya kuitupa na kuwa
kuongeza uchafu.
10. Kama utatumia mifuko kubeba au
kuhifadhia bidhaa mbalimbali , nunua mifuko migumu ambayo inaweza kutumika zaidi
ya mara moja ili kuepuka mlundikano wa mifuko inayotupwa kila siku baada
ya matumizi ya mara moja.
11. Karatasi zilizochapishwa upande
mmoja zinaweza pia kutumika upande wa pili kwa watoto wadogo kuchora au kufanyia
shughuli nyingine zenye uwezo wa kuchangamsha akili zao kabla hazijatupwa na hivyo kufanya zitumike muda mrefu na kupunguza uwezekano wa kununua mpya kwa
matumizi hayo.
Hivyo
taka ngumu ikiwa zitatunzwa na kuhifadhiwa vizuri zinaweza kuleta faida za kiuchumi na kiafya katika jamii husika, ni jukumu la kila
mmjoja kuhakikisha anaishi katika mazingira safi na salama kwa mustakabari wa afya zetu .
No comments:
Post a Comment