TBL: POMBE NI HATARI KWA WAJAWAZITO NA WATOTO



Kampuni ya bia Tanzania (TBL) imesema kuwa inatarajia kuendesha mafunzo kwa wamiliki na wahudumu wa baa na maduka ya kuuzia pombe waelewe athari za kuwauzia pombe wajawazito na watoto.

Meneja Rasilimali watu wa TBL, George Albano alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kiwanda hicho kilichopo Lyunga jijini Mbeya na kujifunza hatua mbalimbali za utengenezaji wa bia.

Alisema matumizi ya pombe kwa wajawazito huleta madhara ya kudumu, kimaumbile na kiakili kwa mtoto atakaezaliwa ambapo pia unywaji pombe wa watoto husababisha watoto kujiingiza katika vitendo viovu.

Alitaja madhara ya kimaumbile yanayoweza kumkuta mtoto ni kutokua vizuri, matatizo ya figo, moyo ambapo pia inaweza kusababisha matatizo ya kitabia ikiwemo ufahamu mdogo na maradhi yanayosababisha mtoto kukosa umakini.

Alisema baada ya kutambua athari hizo, TBL imekusudia kutoa mafunzo kwa wamiliki, wahudumu wa baa na maduka ya kuuzia pombe na kwamba wanaamini wakipata elimu hiyo watakataa kuwauzia pombe wajawazito na watoto.

Aidha, Albano alisema wapo baadhi ya madaktari ambao wamekuwa wakishauri wajawazito kunywa kiasi kidogo cha pombe, Hata hivyo alisema kitaalamu haijathibitika kiwango cha pombe kinachofaa kwa mjamzito na kwamba wanachowashauri ni kwamba wasitumie kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, mtu anapokunywa pombe humfikia mtoto kupitia kondo la nyuma na pombe inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto huathiri uwezo wake wa kupata chakula, virutubisho na hewa ya oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine.




No comments:

Post a Comment