Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), limevisimamisha viwanda viwili vya kutengeneza mikate vya Shoprite na
Sakina Bakery vyote vya jijini Arusha kutokana na kuzalisha mikate bila kuwa na nembo ya ubora,
inayotolewa na shirika hilo.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na maofisa wa TBS, baada ya
kukagua viwanda hivyo na kukuta vikiendelea na uzalishaji wa mikate ambayo
haina alama ya ubora inayotolewa na TBS.
Mwanasheria wa TBS , Babtister Bitaho, akiwa ameambatana
na Mkaguzi, David Ndibalima na Ofisa uhusiano, Rhoida Andusamile, waliendesha
ukaguzi wa viwanda vya mikate jijini Arusha jana na kubaini idadi kubwa ya
mikate inayouzwa ubora wake haujathibitishwa na TBS.
Bitaho alisema sheria ya viwango namba 2 ya mwaka 2009,
inakataza kusambaza bidhaa za vyakula bila kupewa alama ya ubora na TBS.
“Sheria ipo wazi kuwa mtu atakayekutwa anazalisha bidhaa
za vyakula bila kuwa na alama ya TBS, adhabu yake ni faini kati ya Sh50 milioni
hadi Sh100 milioni,” alisema Bitaho.
Ofisa uhusiano wa TBS, Andusamile alisema TBS imeanza
ukaguzi wa viwanda vya mikate ambayo haina ubora na kwamba hatua hiyo imekuja
baada ya kubaini, kuwepo kwa mikate mingi ambayo haina ubora ulioidhinishwa na
TBS.
Alisema kwa sasa kuna viwanda 15 tu vya mikate
vilivyosajiliwa na TBS na viwanda vingine vimekuwa vikizalisha mikate kinyume
na sheria.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment