UGONJWA WA KIPINDUPINDU WALIPUKA, FAHAMU JINSI YA KUJIKINGA



Hivi karibuni ugonjwa wa Kipindupindu umeripotiwa na vyombo vingi vya habari hapa nchini kuwa umelipuka katika wilaya ya Kyela na kuua watu wawili na 39 wakiwa wamelazwa.

Taarifa zinasema ugonjwa huo umeibuka wilayani humo wiki mbili zilizopita ukisadikika kuanzia katika Kijiji cha Ngonga na kisha kusambaa hadi Kilwa

Kutokana na hofu ya kupata maambukizi kwa wananchi wengine, serikali imepiga marufuku mikusanyiko ikiwemo ya harusi, kipaimara, ngoma, michezo na sikukuu inayosherehekewa kila mwaka ya wakulima.

Ili kujikinga na maambukizi ya ugojwa huu hatari ambao huua ndani ya masaa machache baada ya maambukizi, nimeamua kukuletea darasa kwenye Simu na kompyuta yako, kwani naamini nikikufundisha wewe basi nitaisaidia jamii yako yote na watanzania kwa ujumla kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huu.

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuhara unaosababishwa na vimelea vya bacteria viitwavyo Vibrio cholerae, aina ya 01 au 0139. Muda wa kupevuka kwa ugonjwa huu ni masaa mawili hadi matano.

NJIA ZA MAAMBUKIZI

Kwa kawaida kipindupindu huambukiza kwa njia ya maji au vyakula, watu wote watoto na watu wazima wanaweza kuambukizwa.
Milipuko mipya inaweza kutokea ghafla sehemu yoyote ulimwenguni ambapo mgao wa maji, udhibiti afya kwa kuondoa maji machafu na takataka, usalama wa vyakula, na usafi wa kiafya usiotosheleza.

DALILI:

1)      Watu walioambukizwa wanahara maji maji kwa kasi
2)      10-20% ya hawa watu huendelea kuharisha sana pamoja na kutapika.

Kama wagonjwa hawa hawapati matibabu yanayofaa na kwa haraka, upotevu wa kiasi kikubwa cha maji na chumvi mwilini unaweza kusababisha kuishiwa na maji mwilini na kifo ndani ya masaa machache.

EPIDEMIOLOJIA

Vifo kutokana na ugonjwa huu katika bara Afrika ni takriban 5% ya magonjwa yote, kiasi cha wagonjwa wanaokufa kwa wale wasiopata matibabu inaweza kufikia 30-50%. Matibabu ya haraka bila kusita ni muhimu sana (kimsingi ni urudishaji wa maji mwilini) na kama ni matibabu bora yanayofaa, idadi ya watu wanaokufa kwa kipindupindu iko chini ya 1%.

MAZINGIRA HATARISHI

Hatari kubwa ya kutokezea mlipuko ni kwenye sehemu wanapokaa watu wengi mno na kwenye kambi za wakimbizi ambapo hakuna utaratibu mzuri wa udhibiti wa afya, ambapo hakuna maji safi na salama na ambapo kuna ongezeko la maambukizi baina ya watu.

JINSI YA KUJIKINGA

1.  Ondoa maji machafu na takataka kwenye makazi yako
2.  Jenga choo bora kisichoruhusu kuingia na kutoka kwa inzi
3.  Hakikisha unakunywa maji yaliyochemshwa na kula chakula kikiwa cha Moto
4. Osha mikono yako kwa sabuni kabla ya kula Chakula
5. Hakikisha unaosha mikono yako kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka chuoni  
6. Hakikisha unaielimisha jamii yako juu ya kujikinga na Kipindupindu

TAHADHARI

Hakikisha unawahi Hospitalini mapema pale tu unapojisikia kuwa na Dalili za kipindupindu kama zilivyotajwa hapo juu!


No comments:

Post a Comment