Imedondoshwa kutoka Gazeti la Mwananchi la leo
Unapotembea mchana hasa mijini
haikuchukui dakika tano kuweza kuona aina mbalimbali za mipira ya kiume
(kondomu) katika maduka yakiwamo ya kawaida, pia yale ya dawa.
Kondomu hizo zimetengenezwa kwa sura na
maumbile, rangi mbalimbali tofauti ambazo baadhi yake kwa hakika
zinavutia kuzitazama.
Hadi sasa, zipo zenye harufu au marashi
anuwai kama yale ya ndizi, zabibu, chokoleti na hata zile zenye harufu ya Big
G.
Katika nchi zilizoendelea zikiwamo za
Ulaya na Marekani, wataalamu wanaeleza kuwa zipo zile zenye mtetemo maalumu kwa
ajili ya kuliongezea ladha tendo la ndoa.
Pia, zipo zenye majina ya watu
maarufu kama vile, ‘Obama Condom’ ambayo ina picha ya rais huyo wa Marekani
ikionyesha alama ya dole gumba na za Sir Richard.
Lakini, pamoja na kuwepo kwa
kondomu zenye picha za watu maarufu kama Obama, utafiti umebaini kuwa ni asilimia tano tu ya wanaume duniani
ndiyo hutumia mipira hiyo.
Utafiti huo uliochapishwa karibuni na
Shirika la Afya Duniani (WHO) umebaini kuwa wanaume wengi duniani kote
hawapendi kuvaa kondomu, hivyo kukinzana na hali halisi ya changamoto za
afya duniani, ambapo watu milioni 2.5 huambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU)
kila mwaka, zaidi katika nchi za Afrika.
Nchini Marekani, Taasisi ya Bill na
Melinda Gates imeandaa mashindano ya kutengeneza kondomu zitakazompa ladha ya
kipekee mwanaume na mwanamke ili kuongeza matumizi ya kinga hiyo.
Lengo ni kuhakikisha kuwa mimba za
utotoni pamoja na magonjwa ya zinaa hasa Ukimwi vinapungua.
“Kupungua kwa ladha ya tendo la ndoa
ndicho chanzo cha watu kutopenda kuzitumia. Sasa tunafanya juhudi kuhakikisha
zinatumiwa,”anasema ofisa mipango wa taasisi hiyo, Steven Ward.
Mshauri wa Kiufundi wa Afya ya Uzazi wa
Marekani, Jeff Spieler, anasema anatamani iwapo zingeundwa kondomu zinazoongeza
raha ya tendo la ndoa na kulifanya tendo liwe bora zaidi kuliko bila kinga
hiyo.
“Yaani, kondomu iwe nzuri zaidi kuliko
kutenda tendo hilo bila kinga hiyo. Haitakuwa kama kuoga wakati umevaa
koti la mvua,” anasema Spieler.
Taasisi hiyo imeahidi kutoa donge
nono kwa kampuni au wabunifu binafsi watakaounda kondomu ambayo baada ya
kufanyiwa majaribio itaonyesha kuwa na matokeo mazuri.
Hata hivyo, Spieler anasema, mchakato
huo utakuwa mgumu kwani katika hali ya kawaida tendo lenyewe huweza kuwa baya
kwa siku hiyo, hivyo kumfanya mtumiaji kuhisi kondomu hiyo haina ubora.
Hii si mara ya kwanza kwa kondomu
kubuniwa kwani wataalamu wameshawahi kuunda mipira hiyo lukuki kama vilezile za
Ice Cream na ‘Pleasure Plus, zenye plastiki nyembamba ambayo mtumiaji
akivaa huwa ni kama hakuvaa chochote .
Hata hivyo, pamoja na aina hizo lukuki,
bado watumiaji ni wachache na wanalalamika zina kasoro kadhaa kama kubana,
kuunguza au kuchomoka wakati wa tendo.
Mapema mwaka jana, utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kinsley ulibaini kuwa nusu ya
wanaume duniani hawajui jinsi ya kuvaa mipira ya kiume (kondomu) hali
inayochochea kuenea kwa maambukizi ya Ukimwi.
Ilibainika kuwa wengi huivaa vibaya kwa
kuigeuza, kuivaa nusu, kuitoboa wakati wa kuvaa na kuitoa kabla ya wakati.
Mpaka sasa, aina mbili za kondomu,
Morigami na ‘Pronto for Secs’, zipo katika majaribio ya kitabibu na kwa
watumiaji wake.
Hata hivyo taasisi hiyo ilionyesha
wasiwasi wa mafanikio ya uvumbuzi wa kondomu hizo katika nchi zilizoendelea
ambazo zipo katika mrengo wa kitamaduni.
‘Katika nchi nyingine, mwanamke akibeba
kondomu anaonekana kama ni kahaba, lakini kadiri maambukizi yanavyoongezeka
nafikiri watajitambua,” alisema.
Hata nchini Tanzania, bado Tume ya
Kudhibiti Ukimwi (Tacaidis) inashirikiana na kampuni katika kuzindua aina
mbalimbali za kondomu ili kuzipa ubora na kuzifanya zipendwe na watumiaji.
Kwa mfano shirika linalotoa elimu ya
afya nchini(PSI) liliwahi kuzindua kondomu yenye sura mpya yenye vidutu.
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti
Ukimwi nchini (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema kondomu ni njia nzuri ya
kuzuia maambukizi mapya iwapo hata hivyo itatumiwa ipasavyo.
Anasema Dk Mrisho kuwa kondomu
zimekuwa zikitumika nchini kwa muda mrefu sasa, ambapo awali zilikuwa
zikitumika kama njia ya kupanga uzazi, na baada ya kugundulika kwa VVU,
zinatumika kuzuia maambukizi.
“Tafiti zilifanyika kitaifa na kimataifa
na kama ilivyothibitishwa na WHO na UNAIDS ni kwamba kondomu zikitumiwa vizuri
zina uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa,” alisema Dk
Mrisho.
Dhana
potofu kuhusu kondomu
Katika nchi zinazoendelea mpaka
sasa bado kuna changamoto kubwa kuhusu kondomu.
Kwa mfano wapo wanaodhani kuwa kutumia
kondomu kunasababisha ugumba jambo linalosababisha wanaume kuacha kabisa
kuzitumia.
Pia, zipo baadhi ya jamii ambazo
watu huazimana kondomu kwa kudhani ni kitu kinachoweza kuazimwa.
Vilevile zipo jamii ambazo wanawake
hukataa wanaume wanapotumia kondomu wakidhani kuwa wanaonekana wao ni makahaba.
Wapo watu wanaovaa mipira hii miwili wakati wa tendo moja, jambo ambalo
ni kosa na linaweza kusababisha maambukizi.
Wengine hudhani kuwa kondomu hubana na
hivyo kuzuia damu kusafiri katika sehemu ya mbele ya mwanaume.
Wataalamu wanaeleza kuwa jambo ambalo si
kweli kwani mipira hiyo hutanuka kwa zaidi ya inchi nane.
Bofya HAPA kutembelea Mwananchi
No comments:
Post a Comment