Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA), Kanda ya
Kaskazini juzi iliteketeza dawa, vyakula na vipodozi vya aina mbalimbali vyenye
thamani ya zaidi Sh6.9 visivyofaa kwa matumizi ya binadamu vilivyokamatwa
kwenye operesheni maalum iliyoendeshwa jijini Arusha.
Meneja wa TFDA, Kanda ya Kaskazini, Damas Matiko alisema
bidhaa hizo zilikamatwa kutoka katika maduka mbalimbali jijini Arusha wakati wa
oparesheni iliyoendeshwa na mamlaka hiyo kati ya Juni 10 na Juni 27, mwaka huu.
“Pamoja na kukosa usajili kutoka TFDA, baadhi ya bidhaa
tulizokamata zilikuwa zimeisha muda wa matumizi, maelezo kuandikwa kwa lugha
isiyoeleweka kwa walaji, kupigwa marufuku nchini na kuharibika vifungashio,”
alisema Matiko.
Meneja huyo alisema shehena iliyokamatwa na TFDA ilikuwa
zaidi ya nusu tani huku vipodozi na dawa zikiwa na idadi kubwa ikifuatiwa na
vyakula vya aina mbalimbali zikiwamo juisi, mivinyo, pombe kali, unga wa sembe
na ngano pamoja na mafuta ya kupikia.
Katika oparesheni hiyo, TFDA ilishirikiana na taasisi na
mamlaka nyingine wakiwamo polisi, wataalamu wa Idara ya Afya na Mazingira kutoka
Jiji la Arusha.
Akiongea na vyombo vya habari, mmoja wa maafisa afya
kutoka jiji la Arusha aliwaasa wananchi kuwa waangalifu katika manunuzi ya
bidhaa wanazozitumia ikiwa ni pamoja na kuangalia muda wa kuisha ubora wa bidhaa
hizo (expire date) na kuchunguza nembo za kudhibitisha ubora wa bidhaa kabla ya
manunuzi.
No comments:
Post a Comment