Watafiti kutoka Taasisi ya Chakula, Lishe na Afya iliyopo Zurich nchini Switzerland, wameelezea kile walichokiita 'Bakteria wazuri' wanaotoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia maziwa ya mama ambao husaidia kuimarisha afya ya mfumo wa umeng'enyaji chakula na msingi wa kinga ya awali kwa mtoto. Wamesema hii ni sababu nyingine kwamba maziwa ya mama ni bora kuliko vyakula vingine kwa mtoto.
Akiongea na Shirika la habari la Voice of America (VoA), kiongozi wa utafiti huo, Prof. Christophe Lacrox amesema wamebaini aina (strains) ya bakteria wa Bifidobacterium breve na aina nyingine nyingi za bakteria wa Clostridium kwenye maziwa ya mama na kwenye vinyesi vya vichanga na watoto wanaonyonya.
Wataalamu wanaamini kuwa bakteria hao muhimu wanaweza kuimarisha uwiano wa lishe (nutritional balance) kwenye tumbo la mtoto (baby's colon) na kuzuia matatizo ya tumbo (intestinal disorders) kwa mtoto.
Lacroix ameongeza kwamba bado haijafahamika wazi ni jinsi gani hao bakteria muhimu wanavyosafiri kutoka kwenye tumbo la mama kwenda kwenye maziwa, japo kuwa njia mbalimbali za kimaabara zimethibitisha kwamba aina (strains) ya bakteria hao kwa watoto ni sawa kabisa na aina ile inayopatikana kwenye matumbo ya mama.
Lacroix ameuita ugunduzi huu kuwa "unastaajabisha" na kusema tafiti zinazofuata zitalenga kwenye kubaini mfumo (mechanism) wa kusafiri kwa bakteria hao kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye jarida la Environmental microbiology.
No comments:
Post a Comment