UTAFITI WA KUREJESHA MENO MDOMONI KWA KUTUMIA MKOJO WAANZA KUZAA MATUNDA



Utafiti wa karibuni kuhusu meno unaweza kuwa ni habari ya matumaini kwa watu ambao wameng’oa meno mengi mdomoni mwao kiasi cha kuwasababishia shida ya kusaga vyakula vigumu.
Hii inatokana na watafiti wa China kugundua njia ambayo inawezekana ikawa rahisi zaidi ya kumfanya mtu kurejesha meno yaliyopotea mdomoni.
Utafiti huu bado upo kwenye hatua za majaribio kwa wanyama na umeonekana kuleta matumaini, japo wataalamu hao wameona ipo haja ya kuboreshwa zaidi ili uweze kuleta matokeo chanya.
Wanasayansi hao ambao walichapisha matokeo ya utafiti wao kwenye jarida la sayansi la Cell Regeneration, wanasema wakiukamilisha itakuwa ni njia muafaka ya kuwafanya waliopoteza meno yao kwa sababu mbalimbali kuyarejesha.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), wanasayansi hao wametumia teknolojia rahisi ambayo haitahitaji gharama kubwa kupata mali ghafi za kukamilisha mfumo huo.
Wanasema walichogundua ni kwamba mkojo unaweza kutumika kufanikisha kazi hiyo ya kukuza upya meno mdomoni.
Wanasema wamegundua kuwa mkojo unaweza kutumika kuunda seli ambazo zinaweza kutumika kukuza vimelea vinavyofanana kama meno.
Wanasayansi hao wa China waliofanya utafiti huo wanatumai kuwa utafiti huo utaleta mapinduzi katika mfumo wa tiba wa kurejesha kiungo hicho muhimu kwa binadamu.
Walichofanya ni kwamba walichukua mkojo wa binadamu, wakabaini una uwezo wa kusababisha seli kujizalisha.
Kwa sababu hiyo wakakusanya steam seli zinazotoka mwilini kwa njia ya mkojo na kuziweka kwenye maabara.
Mchanganyiko wa seli hizi ulichanganywa na zilizokusanywa kutoka kwa panya ambao hutumiwa kwa utafiti.
Walichokifanya ni kuziweka kwenye mfumo wa utendaji wa mwili wa panya na kuwaendelea kuchunguza kilichokuwa kinaendelea.
Baada ya wiki tatu, wanasema seli zinazofanana na jino zilianza kujitokeza kwenye maeneo ambayo panya alikuwa amepoteza meno.
Yaliendelea kujitokeza na kukua vizuri kiasi cha kuwafanya waamini kuwa matokeo ya utafiti huo ni chanya.
Waliyachunguza meno hayo kwa kina wakabaini kuwa si magumu kama yale ya kawaida. Hata hivyo, meno hayo kutokuwa magumu, kunawapa changamoto ya namna ya kuyarekebisha pengine kwa kuongeza aina nyingine ya kichocheo.
Watafiti wa seli za mwili, wamepokea matokeo hayo kwa furaha wakiamini kuwa ni kupigwa kwa hatua moja mbele katika kutatua tatizo hili sugu duniani.
Wapo pia wanasayansi waliopinga ukuzaji wa seli hizo kwa kutumia mkojo wakisema ipo haja ya kutafuta njia nyingine.

SWALI: Je unadhani njia ya mkojo ni sahihi kutumika kama tiba?


No comments:

Post a Comment