MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
TAARIFA KWA UMMA
18 Julai, 2013
USALAMA WA DAWA AINA YA DICLOFENAC
1. Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) ina jukumu la kulinda na kudumisha afya ya jamii kwa kuhakiki ubora,
usalama na ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
2. Hivi karibuni, TFDA imepokea
taarifa ya kuwepo kwa hofu juu ya usalama wa dawa aina ya Diclofenac kupitia
mitandao ya simu na vyombo vya habari. Kufuatia taarifa hiyo, TFDA inapenda
kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
a. Diclofenac ni dawa iliyoko
kwenye kundi la dawa zinazojulikana kitaalam kama “Non – Steroidal
Anti-inflammatory Drugs” (NSAIDs). Dawa hizi hutumika kutuliza maumivu na
kuondoa uvimbe unaosababishwa na magonjwa mbalimbali. Magonjwa hayo ni pamoja
na magonjwa ya viungo, mifupa, uvimbe wa fizi na maumivu ya kichwa.
b. Mamlaka imesajili dawa ya
Diclofenac kutoka makampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi baada ya kutathmini
ubora, usalama na ufanisi wake. Hata hivyo Diclofenac, kama ilivyo kwa dawa
nyingine, ina madhara yanayofahamika. Kwa baadhi ya wagonjwa Diclofenac inaweza
kusababisha vidonda vya tumbo, kuumwa kichwa, kuharisha, kutapika na kuwashwa
mwili.
c. Pamoja na madhara
yaliyoainishwa hapo juu, hivi karibuni imetolewa taarifa na Mamlaka ya udhibiti
wa dawa ya nchi za Umoja wa Ulaya (European Medicines Agency) kwamba watu wenye
matatizo ya moyo na shinikizo la damu, kisukari, waliowahi kupata kiharusi,
wenye lehemu (cholesterol) nyingi kwenye damu, mshituko wa moyo na wanaovuta
sigara wanaweza kupata matatizo kwenye moyo na mfumo wa damu ikiwa watatumia
Diclofenac kwa kiwango kikubwa na kwa muda mrefu.
3. Kufuatia taarifa hiyo, TFDA
inaendelea kufuatilia madhara yatokanayo na dawa hii kwa kushirikiana na
taasisi nyingine za kitaalam ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Shirika la
Afya Duniani (WHO). Aidha, tunawakumbusha watoa huduma za afya kutoa taarifa za
madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kujaza fomu maalum zinazopatikana
katika vituo vyote vya afya nchini.
4. Mamlaka
inasha+uri watoa huduma za afya nchini na wagonjwa kuchukua tahadhari za
madhara haya hasa kwa watu wenye magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari,
wenye lehemu nyingi kwenye damu na wanaovuta sigara ikiwa ni pamoja na kutumia
dawa mbadala.
5. Vilevile
wananchi wanashauriwa kuepuka matumizi holela ya dawa bila kupata ushauri wa
kitaalam ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Imetolewa na:
Mkurugenzi
Mkuu
Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) – Makao Makuu
S. L. P
77150
Dar-es-Salaam
Tanzania
Simu: +255
22 2450751
+255 22
2450512
Barua pepe:
info@tfda.or.tz
Tovuti:www.tfda.or.tz
No comments:
Post a Comment