TFDA, ATME NA NIMR, KUNA NINI JUU YA UTATA WA MAFUTA YA UBUYU?


Kwanza kabisa napenda kuwakaribisha wasomaji wa blugu hii ili tuweze kujifunza pamoja.

Katika pitapita zangu za kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari nimekutana na habari tofauti tofati zinazohusu Matumizi ya Mafuta ya Ubuyu huku kukiwa na mkanganyiko wa uhalali wa matumizi wa mafuta haya.

Ikumbukwe kwamba siku za hivi karibuni kumeibuka wajasiriamali wengi wanaouza mafuta ya ubuyu huku na kule ambao wamekuwa wakitumia kigezo cha Tiba kama mhimili mkubwa katika matangazo ya biashara yao, watu mbalimbali wamekuwa wakivutiwa sana na mafuta haya hasa ukizingatia wanasema “yanatibu magonjwa” Ooooh yes, hata mimi nilishawahi kuvutiwa kwakuwa kulikuwa hakuna elimu yoyote iliyopingana na matumizi yake na elimu iliyokuwepo ni ile iliyotolewa na wauzaji wa mafuta hayo ‘umuhimu wa mafuta ya Ubuyu kiafya’.

Ni kama juma moja hivi lililopita, nilipata habari kupitia vyombo vya habari hapa nchini  kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imepiga marufuku matumizi ya mafuta ya Ubuyu kwa sababu yaligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha tindikali inayojulikana kwa Kimombo kama Cyclopropenoic fatty acids inayoweza kuathiri vimeng’enyo vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini, na kuongeza kwamba ili yaweze kukidhi vigezo vya ubora na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji wakati wa usindikaji kwa kuyachemsha kwenye joto lisilopungua 1800C kwa muda wa masaa nane na kwamba kwa sasa hakuna aina ya usindikaji hapa nchini unaofanyika yenye uwezo wa kuondoa tindikali hiyo ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya mbegu za ubuyu. Niliposikia hii habari nikajisemea kimoyomoyo “TFDA imefanya jambo jema sana kuitahadharisha Jamii yetu ya Tanzania kwani hata wazungu hatua kama hizi huwa wanaziita ‘precautionary principal’”.

Siku chache baada ya tamko hilo la TFDA nikasoma gazeti lingine, gazeti hili lilibeba ujumbe wa Chama cha Watabibu wa Dawa za Asili Tanzania (ATME) kuhusu Tamko la TFDA. Mratibu wa ATME alisema taarifa zilizotolewa na TDFA kuhusu matumizi ya mafuta ya ubuyu zinaweza kuleta madhara kwa jamii kwakuwa wamekuwa wakiyatumia zaidi ya miaka 20 kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo na viusi vya ukimwi, na kudai mafuta hayo yamekuwa yakiwasaidia sana huku akiongeza kwamba wanayo kumbukumbu ya wagonjwa waliowahi kutibiwa na mafuta hayo na hawajawahi kusikia malalamiko yoyote juu ya madhara ya mafuta hayo. Mmmh! Mpaka hapa nikajiuliza “ina maana mpaka TFDA wanatoa tamko hilo kwa umma, hawakuwasiliana na hiki chama ambacho ni muhimu sana kwenye tiba za Asili na kujaribu japo kufanya tathmini ya utafiti wake na wagonjwa waliotibiwa na ATME ili wapate cha kuwadhibitishia wananchi?”

Pamoja na matamko hayo ya TFDA na ATME kwenye vyombo vya habari kuonekana kuwa na viashiria vya kupingana, leo nimesoma habari nyingine tena kwenye gazeti Fulani lililoripoti kwamba Serikali kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya binadamu (NIMR) imesema bado haijabaini madhara yoyote ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya Mafuta ya Ubuyu na ipo katika utafiti ili kubaini kama kuna kiwango kikubwa cha Tindikali ya mafuta kilichotajwa na TFDA (Cyclopropenoic fatty acids). Mpaka hapa nikagundua kwamba kumbe TFDA imetoa tamko bila kuwashirikisha wadau wa Tiba asilia…! japo hawajafanya vibaya kuitahadharisha jamii juu ya viashiria vya uwepo wa Tindikali ya mafuta kwenye mafuta ya ubuyu lakini kwanini vyombo hivi vitatu havikukaa pamoja kujiuliza mustakabali wa Jamii yetu kisha wakaja na Tamko moja lililonyooka!?????

Je tumwamini nani kati ya TDFA na ATME  juu ya uhalali wa matumizi ya mafuta ya ubuyu ikiwa NIMR bado ipo kwenye utafiti???



No comments:

Post a Comment