Na Rose Riwa
Habari wasomaji wa ‘AFYA
YA MAZINGIRA’, natumaini nyote ni wazima wa afya na mnahifurahia siku yenu. Kwanza
nianze kwa kuwatakia ndugu zetu waislamu mfungo mwema wa ramadhani na maandalizi
mazuri ya sikukuu ya IDD, pia kwa kuwapa hongera wasomaji wetu wote kwa
kumaliza kazi kwa wale ambao wametoka makazini au kwenye shughuli mbalimbali za
kuingiza kipato kwa siku, ngoja nisiwachoshe na niende moja kwa moja kwenye
mada ya leo ambayo walengwa ni wanawake, wanaume wenye wake au watoto wa kike
na wazazi wenye watoto wa kike waliobalehe.
Kumekuwa na ongezeko
kubwa la magonjwa ya mfumo wa mkojo (UTI) na uzazi kwa wanawake, hii
inasababishwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosa uelewa sahihi wa kanuni za
afya na usafi wa mwili pamoja na mazingira yanayomzunguka mwanamke. Mada za
usafi wa mwanamke ni pana sana siwezi kumaliza kusema kila kitu, hivyo leo
nitajikita zaidi katika matumizi sahihi ya pedi na mambo ya kuzingatia kabla ya
kunua pedi. Wadada wengi wamekuwa wakitumia pedi na kuziacha zikizagaa mitaani
hali inayofanya nijiulize kama tu ameshindwa kujua sehemu sahihi ya kuhifahi au
kutupa pedi aliyotumia yeye mwenyewe, Je anauelewa upi katika matumizi sahihi
ya pedi hizo kabla hajazitumia? Somo la leo nitajikita katika njia sahihi ya kuchagua na kutumia
pedi, makosa yanayofanywa katika matumizi ya pedi na ushauri juu ya matumizi
sahihi ya pedi na vitambaa kwa wale wanaovitumia.
Yafuatayo ni makosa yanayofanywa katika
uchaguzi na matumizi ya pedi kwa wanawake:
1. Kutonawa
mikono kabla na baada ya kutumia pedi. Mikono hushika sehemu mbalimbali hivyo kuna uwezekano ikawa na vimelea
vinavyosababisha magonjwa kwa hiyo kushika pedi bila kunawa mikono kwa sabuni
kunaweza kuhamisha vimelea hivyo kutoka mikononi na kwenda kwenye pedi
inayotegemewa kuvaliwa.
2. Kutunza pedi bafuni au chuoni. Wadada wengi
hupendelea kutunza pedi zao chooni/bafuni. Vyumba vingi vya choo/bafu havina
mwanga wa kutosha na kuwa na unyevunyevu hali inayoweka mazingira mazuri ya
ukuaji wa vimelea vya magonjwa kama bacteria na kitendo cha kutunza pedi katika
sehemu hizo kunaweza kusababisha kuhama kwa vimelea hao kutoka bafuni/chuoni kwenda
kwenye pedi isiyovaliwa na kupelekea pedi hizo kuwa na vimelea vya magonjwa na mwanamke anakuwa
katika hatari za kupata maambukizi.
3. Kutoangalia muda wa matumizi wa pedi
kabla ya kutumia au baada ya kuzihifadhi kwa muda mrefu hali inayopunguza
kiwango cha ufanisi cha pedi sababu ya kuisha kwa muda wake wa matumizi.
4. Kununua pedi zinazouzwa kiholela kwa
njia ya utangazaji na za bei rahisi (promotion) ambazo baadhi zimeonekana
kutengenezwa kwa malighafi zilizo chini ya kiwango au kukaa kwa muda mrefu hivyo
kuuzwa kwa bei rahisi ili zitoke na kutumika haraka kabla ya kuisha muda wake.
5. Kutumia pedi ambazo zipo katika
majaribio maalum. Kama tunavyojua kuna kila aina za pedi mpya katika soko kwa kadri siku
zinavyozidi kwenda na baadhi ya pedi huingizwa sokoni kinyemela
pasipo tafiti za kutosha na bila hata kuthibishwa na mamlaka husika.
6. Kutumia pedi kwa muda mrefu. Wanawake wengi
hususani katika nchi zinazoendelea huwa
hawamudu kutumia pedi moja kwa muda wa masaa mawili kama inavyoshauriwa na
wataalamu hivyo kujikuta katika hatari ya kupata magonjwa ya mfumo wa mkujo na
njia za uzazi .
7. Kupendelea pedi zenye uwezo mkubwa wa kufyonza
unyevunyevu ili ivaliwe muda mrefu pia ni tatizo sababu kwa kadri muda wa kuvaa
pedi moja unapozidi kuongezeka na hatari za maambukizi ya magonjwa pia inazidi
kuongozeka.
Wanawake wanashauriwa
kufanya yafuatayo ili kuhakikisha usalama wa afya zao :
1. Kunawa mikono vizuri kwa sabuni kabla ya
kugusa pedi ambayo unatarajia kuivaa na baada ya kuvaa kunawa tena mikono
vizuri.
2. Kutohifadhi pedi bafuni au chuoni au
sehemu yote yenye unyevunyevu na isiyo na mwanga wa kutosha ili kutotengeneza
mazingira ya kukua kwa vimelea vya magonjwa ndani ya pedi.
3. Kuangalia kwa makini muda wa matumizi ya
pedi kabla ya kununua au baada ya kutunza pedi kwa muda muda mrefu ili kuepuka
kutumia pedi zilizopita muda wake wa matumizi.
4. Kuepuka kununua pedi zinazouzwa kiholela
na zisizothibitishwa na TBS na mamlaka nyingine zenye dhamana ya kuangalia
ubora wa pedi hizo. Mwanamke anatakiwa
kuangalia nembo ya uthibitisho wa mamlaka hizo na kujiridhisha kuhusiana na
usalama wa pedi hizo kabla hajanunua.
5. Kubadilisha pedi kila baada ya masaa mawili, kama tunavyojua
damu ni moja wapo ya chakula kizuri sana kwa vimelea vya magonjwa kama bacteria
,unyevunyevu unaosababishwa na kuvaa
pedi kwa muda mrefu pia unapelekea ustawi wa bacteria hao na joto ambalo lipo katika maumbile ya ndani
ya mwanamke vikiungana kwa pamoja vinatengeneza mazingira mazuri ya ukuaji wa
bacteria , hivyo wanawake wanashauriwa kutovaa pedi hizo kwa muda usiozidi
masaa mawili ili kuepuka mazingira hayo.
6. Kuchagua aina sahihi inayokutosha ina
kuepuka pedi zinazobana sana kupita kiwango sababu zinaweza pia kukufanya usiwe
huru na kutengeneza joto la ziada na
michubuko katika maumbile ya mwanamke,hivyo mwanadada unashauriwa kutumia pedi
itakayokukaa vizuri(isilegee sana wala kuachia sana)
7. Kwa wadada wanaotumia vitambaa badala ya
pedi ni muhimu pia kuzingatia kanuni za kiafya na usafi kabla na baada ya
kutumia vitambaa hivyo kama vile kuchagua kitambaa angavu ,kukiloweka na
kukifua vizuri, kuanika kwenye sehemu yenye mwanga wa jua wa kutosha na upepo
wa kutosha pasipo na unyevunyevu ,kupiga pasi kabla ujakihifadhi na kabla ya
kutumia ili kuuwa vimelea vya magonjwa na kuvitunza sehemu nzuri ambayo haina
unyevunyevu, penye hewa na mwanga wa kutosha na mwisho ni kubadilisha kitambaa hicho kila baada ya masaa mawili
pamoja na kunawa mikono vizuri kabla na baada ya matumizi ya vitambaa hivyo.
AHSANTE!
No comments:
Post a Comment