Na Goodluck Mselle Bsc EHS-EHO Kinondoni Municipal
Council Dar-es-salaam
(source: Mwananchi,15 August 2013)
Uchafu wa hali ya juu…usiofaa kwa kutazama, wala
kuutumia kufanya kazi fulani, umegundulika kuwa na manufaa lukuki kwa matumizi
ya binadamu. Uchafu huo si mwingine bali ni kinyesi cha binadamu pamoja na
mkojo.
Mfumo wa usafi wa mazingira ya kiikolojia
hautiliwi maanani hapa nchini, pamoja na kufafanuliwa kwa kina na wataalamu
mbalimbali, lakini bado imekuwa ni vigumu kwa Watanzania kuitilia maanani na
kuitumia kwa tija.
Barani Asia, taka mwili zimekuwa zikihifadhiwa na
kufanyiwa utafiti kwa miaka zaidi ya 1,000, huku mfumo huo ukilindwa katika
vifungu vya sheria ya kutunza taka ya mwaka 1988, Korea ya Kusini.
Kitaalamu mfumo huo unajulikana kama Ecological
Sanitation System, ambao unatumia taka mwili za binadamu na kuzirejesha katika
matumizi yenye thamani huku ukitunza mazingira.
‘Taka mwili’ zinafaa kwa nishati
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Profesa Fredrick Mwanuzi anasema kama usimamizi wa mazingira
utazingatiwa basi ipo haja ya kufanyia utafiti taka mwili kwa ajili ya matumizi
mbalimbali kwa sababu zina manufaa makubwa katika nyanja mbalimbali.
Mwanuzi anasema wakati umefika sasa kinyesi cha
binadamu kichukuliwe kama malighafi badala ya uchafu na kutumia mbolea hiyo kwa
ajili virutubisho vya kilimo, nishati, pamoja na dawa za binadamu.
“Kilo 25 hadi 50 za kinyesi huzalishwa na mtu
mmoja kwa mwaka, hii ni sawa na kilo 0.55 nitrogen, 0.18 phosphorus na 0.37
potassium, vilevile binadamu huzalisha kiasi cha lita 400 za mkojo kwa mwaka
ambazo huwa na kg 4.0 nitrogen, 0.4 phosphorus na 0.9 za potassium,” anasema.
Wataalamu wa mazingira nchini Tanzania walijaribu
‘taka mwili’ kuzifantia mchakato wa kitaalamu ili kuwa malighafi, walichagua
eneo la Majumba Sita jijini Dar es Salaam lengo kubwa likiwa ni kuzuia kinyesi
kinachotoka chooni kuchafua maji ambayo yapo ardhini.
Mtaalamu wa mazingira Esnati Chaggu alifanya
utafiti na kugundua kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam wanatumia vyoo vya shimo ambavyo vinachafua maji yaliyomo ardhini huku
watu wengi wanategemea maji ya visima vyenye urefu zaidi ya meta 6.75 pamoja na
mabomba ambayo huathiriwa na kinyesi kinachofukiwa ardhini. “Maji yaliyoko
ardhini yanaathiriwa na aina ya vyoo ambavyo Watanzania wanavitumia, asilimia
90 hutumia vyoo vya shimo.
“Tulichagua eneo la Majumba Sita ambalo lina
asilimia kubwa ya visima vyenye kina kifupi na wakazi wengi wanatumia vyoo vya
shimo na wengine hawana kabisa na wanajisaidia vichakani,” anasema.
Kutokana na mazingira hayo walibuni namna ya
kuhifadhi kinyesi cha binadamu kwa manufaa na pia kutunza mazingira hasa maji
ambayo yalisababisha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na
kuharisha.
“Tulibuni teknolojia ya Ecosan, (usafi wa
mazingira) ambayo vyoo vilitumika katika kudhibiti taka mwili, vyoo vya aina
mbili viligunduliwa cha kwanza ni kile cha kuchuchumaa na kukaa ambavyo
viliwekewa sehemu ya kutenganisha mkojo,” anasema Chaggu.
Anafafanua kwamba mkojo ulielekezwa kupita katika
bomba kuelekea katika chombo cha plastiki chenye ujazo wa lita sita ambacho
huwekwa nje ya choo na kuchimbiwa ardhini, taka hizo huhamishwa baada ya siku
13 baada ya chombo kujaa wakati huo kinyesi hukusanywa sehemu nyingine moja kwa
moja kutoka katika choo cha kuchuchumaa.
“Lakini ili yabaki maji machache katika kinyesi
majivu humwagiwa katika shimo la choo kila baada ya kujisaidia, njia hii ni
bora katika kupunguza harufu na maambukizi ya magonjwa,” anasema.
Aina ya pili ni choo cha kukaa cha 96 Ecosan au
‘Ecological Sanitation’. Dk Mwanuzi anaeleza kwamba taka mwili, kinyesi kigumu
hutenganishwa na mkojo.
“Hii ina usalama zaidi kwa matumizi bila wadudu
wabaya. Ukitenga mkojo una bei nzuri sokoni kwa kuwa unauza kama mbolea ya
UREA,” anasema
Kilimo
Kwanza
Professa Mwanuzi anasisitiza matumizi ya kinyesi
cha binadamu kwa wakulima hasa katika mkakati wa Kilimo Kwanza na nishati kwa
wakazi wa vijijini.
Anasema kinyesi cha binadamu pia kinatumika
kutengeneza nishati ya gesi ambayo kitaalamu huitwa ‘biogas’ ambayo inafaa
zaidi kuendeshea injini, umeme na kupikia.
“Gesi hii ina manufaa kwa familia zilizoko
vijijini kwa ajili ya kuzalisha umeme,” anasema.
Anasema asilimia kubwa ya wakazi wa Kanda ya
Kaskazini Arusha na Kilimanjaro wanatumia mbolea ya asili ya wanyama kwa ajili
ya mimea kama kahawa na migomba na mbolea hiyo imeleta mafanikio makubwa katika
kilimo.
No comments:
Post a Comment